Writen by
sadataley
1:17 PM
-
0
Comments
- “Asema wasithubutu kuingia huko mtafungwa
NA MWANDISHI WETU
DAWA za kulevya ni moja kati ya vitu
vyenye madhara makubwa ambavyo vinachangia kuporomosha uchumi wa Taifa
kwa sababu yanaathiri vijana wengi ambao ndiyo nguvu kazi.
Hata hivyo dawa za kulevya zimekua
zikiigharimu Serikali kwa kutumia fedha nyingi katika kupambana na
athari zitokanazo na matumizi dawa hizo, hivyo imewataka wananchi na
jamii kiujumla kutojihusisha na biashara hiyo haramu.
Mbali na dawa hizo kulisababishia Taifa
madhara ya kiuchumi na kiafya, pia biashara hiyo ya dawa za kulevya
inachafua na kushusha hadhi ya Tanzania kimataifa.
Madhara ya kiafya yanayosababishwa na
matumizi ya dawa za kulevya ni pamoja na kuathirika kwa mfumo wa fahamu
kwa mtumiaji ikiwa ni pamoja na kuchanganyikiwa, kuwa na ulevi
uliopindukia na hatimaye kusababisha kifo kama mtumiaji atazidisha
matumizi.
Katika kuhakikisha biashara hiyo
inakomeshwa Serikali imeunda Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za
Kulevya nchini ambayo ndiyo inayoongoza mapambano hayo.
Jumatano ya Machi 22, mwaka huu akiwa
nchini Mauritius, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alizungumza na Watanzania
waishio nchini huko katika mkutano alioutisha kwenye hoteli ya Meridien
mjini Port Louis.
Akizungumza na Watanzania hao aliwataka
wajiepushe na masuala yahusuyo dawa za kulevya. Aliwataka Watanzania
wote wanaoishi nje ya nchi wazingatie sheria za Taifa husika na kamwe
wasijihusishe na biashara haramu ya dawa za kulevya.
“Vita ya dawa za kulevya ni kubwa, hata
hivyo Serikali tunaendelea kupambana nayo. Nchi ilikuwa inapoteza vijana
ambao walikuwa wamejiingiza katika biashara haramu ya dawa za kulevya.
Nawaomba msithubutu kuingia huko mtafungwa,” alisema.
Alisema katika kudhibiti biashara hiyo
haramu ya dawa za kulevya Serikali iliamua kuunda Mamlaka ya Kuzuia na
Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na inafanya kazi vizuri. “Na
tutakamata kila mtu anayejihusisha na biashara hiyo bila kujali cheo,
uwezo na mamlaka aliyonayo,”.
Aliongeza kuwa mamlaka hiyo inafanya
kazi ya kutafuta wazalishaji, watumiaji na wafanyabiashara, lengo likiwa
ni kuokoa vijana ambao wameshindwa kutimiza ndoto zao kutokana na
madhara waliyoyapata baada ya kutumia dawa za kulevya.
Waziri Mkuu alisema kuna Watanzania
wengi wamefungwa katika magereza mbalimbali duniani na wengine
wamehukumiwa kunyongwa baada ya kuthibitika kuwa wanajihusisha na
matumizi, usafirishaji na uuzaji wa dawa za kulevya, hivyo aliwataka
wawe mabalozi wazuri wa Tanzania kwa kujiepusha na dawa za kulevya.
Akizungumzia idadi ya watu ambao hadi
sasa wamekwishakamatwa katika nchi mbalimbali, Waziri Mkuu alisema
takwimu za jumla zinaonyesha kuwa Watanzania 515 wamekamatwa na kufungwa
gerezani kwa makosa ya kujihusisha na biashara ya dawa ya kulevya.
“Nchini China Watanzania walioko
magerezani ni zaidi ya 200; Brazili kuna Watanzania 12; Iran wako
Watanzania 63; Ethiopia Watanzania saba na Afrika Kusini wako Watanzania
296,” alisema.
Waziri Mkuu aliongeza kwamba “Dawa za
kulevya ni hatari sana kwa usalama na ustawi wa Taifa letu. Vita hii
inayopiganwa sasa dhidi ya uagizaji, uzalishaji, usambazaji na matumizi
ya dawa za kulevya ni kubwa. Sote kwa pamoja tunapaswa kuunga mkono
jitihada hizo,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa taarifa zililizopatikana
ndani ya Jeshi la Magereza Tanzania hadi Machi 26, mwaka huu kulikuwa na
wafungwa 512 wanaotumikia vifungo vyao katika magereza mbalimbali
kutokana na makosa yanayohusiana na dawa za kulevya, ambapo kati yake
wanaume ni 491 na wanawake 21.
Mbali na wafungwa pia kuna mahabusu
1,284 wanaoshikiliwa kwa tuhuma za kujihusisha na utumiaji, usafirishaji
na uuzaji wa dawa za kulevya, ambapo kati yao wanaume ni1,166 na
wanawake ni 118.
Katika hatua nyinngine, Waziri Mkuu
aliwataka Watanzania hao walioko nchini Mauritius kujenga mshikamano wa
pamoja na wawe na uzalendo na nchi yao. Pia wawe mabalozi wazuri wa
kutangaza vivutio vya Taifa.
Alisema ni vema wakatumia fursa
walizonazo katika kutafuta wawekezaji na kuwashawishi waje nchini na
kuwekeza kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za viwanda, uvuvi, nishati na
utalii.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na
Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohammed
aliwaomba Watanzania hao wazidishe mshikamano miongoni mwao kwa kuwa
umoja wao ndiyo nguzo yao.
“Mko hapa kwa ajili ya kutafuta elimu na
wengine mnafanya kazi, shughuli ambazo zitawasaidia kuboresha
maendeleo yenu na Taifa kwa ujumla, hivyo nawaomba mzingatie
kilichowaleta,” amesema.
Dkt. Khalid aliwahakikishia Wanzania hao
walioko nje ya nchi kuwa Tanzania iko salama na wanaendelea kudumisha
amani na utulivu kama walivyoiacha wakati walipondoka.
Naye Mwenyekiti wa muda wa Umoja wa
Watanzania waishio nchini Mauritius, Bw. Donald Kongwa ambaye ni Ofisa
wa benki ya Standard Chartered nchini Mauritius alimuhakikishia Waziri
Mkuu kwamba kipato wanachokipata watakitumia kwa kuwekeza Tanzania kwa
lengo la kukuza uchumi wa Taifa.
Alisema wanaunga mkono na kupongeza
jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kujenga
uchumi wa viwanda, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, ujenzi wa
miundombinu ya kisasa, ununuzi wa ndege pamoja na kuimarisha uwajibikaji
na nidhamu kwa watumishi wa umma.
Bw. Kongwa alisema Tanzania ina nafasi
kubwa ya kujifunza mambo mbalimbali nchini Mauritius kama namna bora ya
kuendesha kilimo cha miwa kwa sababu nchi hiyo inazalisha zaidi ya tani
600,000 za sukari kwa mwaka na tani 530,000 inauzwa nje ya nchi.”Tutumie
fursa hii kujifunza zaidi ili tuweze kukuza uchumi wetu,”.
Aliongeza kuwa mbali na kujifunza kilimo
cha miwa pia Tanzania inaweza kutangaza vivutio vyake vya utalii nchini
Mauritius ili kuwawezesha watalii wengi wanaoingia nchini humo kuweza
kuvifahamu na hatimaye kuwa nchini. Kwa mwaka Mauritius inapata watalii
zaidi ya milioni moja.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S.L.P 980, DODOMA
IJUMAA, MACHI 31, 2017.
No comments
Post a Comment