Writen by
sadataley
8:07 AM
-
0
Comments
Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un amempongeza Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuchaguliwa tena baada ya kushinda katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni hapa nchini.
Ujumbe uliotolewa na Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini kwa Rais Rouhani umesema: "Kuchaguliwa kwako mara ya pili Mheshimiwa kuiongoza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni ishara ya imani ya hali ya juu na uungaji mkono wa wananchi wa Iran kwako."
Aidha amesema: "Nina imani kuwa mahusiano ya kirafiki ya pande mbili na kadhalika ushirikiano wa Tehran na Pyongyang katika kutetea usalama na amani ya dunia na pia kufikiwa uadilifu wa kimataifa, yataendelea kuimarika zaidi." Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini amemtakia Dakta Hassan Rouhani mafanikio mema katika uongozi wake wa awamu ya pili nchini hapa.
Wakati huohuo serikali ya Pyongyang imethibitisha kufanyia majaribio kombora jipya la balestiki la masafa ya wastani na kuongeza kuwa, kombora hilo lipo tayari kusimikwa na kutumiwa kijeshi. Taarifa liyotolewa na Pyongyang mapema leo imesema kuwa, kombora hilo lililofanyiwa majaribio leo ni aina ya Pukguksong-2 ambalo linatumia mafuta mazito huku likiwa na uwezo wa kushambulia kwa haraka.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kombora la Pukguksong-2 lina uwezo wa hali ya juu wa kulenga shabaha. Hii ni katika hali ambayo Jumapili ya jana pia, Korea Kaskazini ilifyatua kombora lingine la balestiki kuelekea upande wa bahari ya Japan. Kufuatia majaribio hayo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeitisha kikao cha dharura kwa ajili ya kujadili majaribio ya kombora hilo jipya. Kwa mujibu wa habari hiyo, kikao hicho kimeitishwa kwa ombi la Marekani, Korea Kusini na Japan.
No comments
Post a Comment