Saturday, July 8, 2017

Fatou Bensouda, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa mahakama ya ICC
Bunge la Afrika Kusini limepinga hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, kuhusu Afrika Kusini kushindwa kutekeleza wajibu wake kwa mahakama hiyo wa kumkamata Rais Omar Al Bashir alipokuwa nchini Afrika Kusini mwezi Juni mwaka 2015.
Shiphosezwe Masango, Msemaji wa Kamati ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Bunge la Afrika Kusini amesema kwamba, inabidi ikumbukwe kuwa Rais Omar al-Bashir hakwenda Afrika Kusini kwa mwaliko wa serikali ya nchi hiyo, bali alikuwa anahudhuria mkutano wa Umoja wa Afrika.
Amesema kwamba, kama ilivyo kwa Umoja wa Mataifa ambako marais wanahudhuria mikutano muhimu nchini Marekani, lakini hawawezi kukamatwa, kwa sababu huenda nchini humo kwa mwaliko wa Umoja wa Mataifa ni vivyo hivyo ilivyojiri kwa safari ya rais wa Sudan nchini Afrika Kusini.
Msemaji wa Kamati ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Bunge la Afrika Kusini ameonya kuwa, kama Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC itaendelea na msimamo wake kuhusu hukumu hiyo, basi serikali ya Afrika Kusini italichukulia suala la kujitoa kwenye mahakama hiyo kama suala la haraka.
Juzi Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imetangaza kuwa, Afrika Kusini, ilifanya makosa kwa kutomtiA mbaroni Rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan wakati alipofanya ziara nchini humo mwaka 2015.
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi imeshatoa waranti mara mbili wa kukamatwa Rais al-Bashir, mwaka 2009 na 2010. Hata hivyo nchi nyingi hususan za Afrika zimekataa kumkamata na kumkabidhi kwa ICC rais huyo wa Sudan, alipozitembelea nchi hizo.
Parstoday
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment