Saturday, July 8, 2017

Mahakama ya EAC yakataa ombi la Tanzania kuhusu EPA

Baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC
Mahakama ya Haki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, imetupilia mbali kesi iliyowasilishwa na Tanzania kupinga mkataba wa kibiashara kati ya Mataifa ya Jumuiya hiyo na Umoja wa Ulaya EPA.
Mahakama hiyo imekataa kusikiliza ombi la Tanzania kutaka mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutotia saini mkataba huo wa kibiashara.
Tanzania, Uganda na Burundi hazijatia saini mkataba huo kwa madai kuwa hauna maslahi ya mataifa hayo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hata hivyo, tayari Kenya na Rwanda zimetia saini mkataba huo.
Jaji wa Mahakama hiyo Isaac Lenaola, pia hakuizuia Kenya na Rwanda kuendelea na mipango mingine kuhusu mkataba huu.
Uongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hata hivyo umekubaliana kwenda nchini Ubelgiji kuzungumza na viongozi wa Umoja wa Ulaya kuhusu mkataba huu.
Tanzania na Uganda zimekuwa zikipinga mkataba wa ushirikiano wa kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya (EU) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambao kwa kifupi unafahamika kama EPA na zimekuwa mstari wa mbele kuendesha kampeni za kuukataa mkataba huo.
Mkutano wa Tano wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliishauri Serikali ya nchi hiyo kutosaini Mkataba wa Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Nchi za Ulaya (EU) – (EPA) kwa kuwa hauna manufaa kwa nchi ya Tanzania.
Parstoday
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment