Sunday, July 9, 2017

Indhari ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki kwa wakuu wa G-20

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani ametaka kuhitimishwa maafa na mashindano yasiyo na maana ya silaha kote ulimwenguni.
Wahajiri wakilia kwa uchungu katika bahari ya Mediterania wakielekea Ulaya
Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki amewatumia ujumbe wakuu wa kundi la G-20 wanaokutana huko Hamburg nchini Ujerumani akisisitiza kuwa, vita kamwe haiwezi kuwa njia ya ufumbuzi wa matatizo na amezitaka nchi zote duniani kuhitimisha maafa na mashindano ya silaha kote duniani. 
Ujumbe wa Papa Francis kwa viongozi wa G-20 umewataka wakuu wa G-20 kutoa kipaumbele kwa watu maskini na wahajiri bila ya  kubagua nchi, utaifa, dini au utamaduni  wao.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki pia amewataka viongozi wa G-20 kukomesha mizozo ya silaha na mauaji ya halaiki duniani. 
Kundi la G-20 linaundwa na nchi 19 na Umoja wa Ulaya zinazostawi zaidi kiuchumi duniani. Mkutano wa siku mbili wa viongozi wa nchi wanachama katika kundi hilo ulioanza leo huko Hamburg nchini Ujerumani.
Miongoni mwa masuala yanayojadiliwa na viongozi wa G-20 ni mabadiliko ya hali ya hewa, biashara huru, mgogoro wa Korea Kaskazini, utekelezaji wa mpango wa maendeleo endelevu wa Umoja wa Mataifa, mgogoro wa wakimbizi na njia za kupambana na ugaidi.
Parstoday
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment