Sunday, July 9, 2017

Wanasiasa wawili kuchuana na Kagame katika uchaguzi wa rais Rwanda

Rais Paul Kagame anayepewa nafasi kubwa ya kushinda kiti cha uraias katika uchaguzi wa mwezi ujao nchini Rwanda
Rais Paul Kagame wa Rwanda anatarajiwa kuchuana na wanasiasa wawili katika uchaguzi wa mwezi ujao wa Rais nchini Rwanda, huku duru mbalimbali zikimtabiria ushindi mkubwa.
Hiyo ni baada ya Tume ya Uchaguzi nchini Rwanda, kuwaidhinisha wagombea wawili wa upinzani kupambana na rais Paul Kagame wakati wa Uchaguzi Mkuu mwezi ujao, baada ya wagombea wengine akiwemo mwanamke pekee kushindwa kukamilisha masharti.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Tume ya Uchaguzi  ya Rwanda Profesa Kalisa Mbanda ni kuwa kuwa, wanasiasa hao wawili wa upinzani waliokidhi vigezo vya kuwania urais ni pamoja na Frank Habineza, kutoka chama cha Democratic Green Party na mgombea binafsi Philippe Mpayimana.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, Gilbert Mwenedata, Fred Barafinda Skikubo na mwanamke wa pekee Diane Rwigara hawakufanikwia kuidhinishwa baada ya kushindwa kupata saini 600 za wapiga kura kama inavyotakiwa kikatiba.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, kampeni rasmi za uchaguzi huo, zinatarajiwa kuanza tarehe 14 mwezi huu na kumalizika Agosti tatu ikiwa ni siku moja kabla ya kufanyika uchaguzi wenyewe.
Duru za kieneo na kimataifa zinamtabiria ushindi mkubwa Rais Kagame katika uchaguzi huo wa mwezi ujao hasa kutokana na kutokuweko upinzani mkali. Hatau ya baadhi ya wapinzani kutangaza kumuunga mkono Rais Kagame imepelekea kudhoofika upinzani na hivyo kukiandalia chama tawala cha RPF  fursa ya kuendelea kutawala nchini humo.
Parstoday
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment