Friday, September 29, 2017

Ripoti: Wakimbizi wa Burundi wanashinikizwa kurejea nyumbani, lakini hali bado si shwari

Ripoti: Wakimbizi wa Burundi wanashinikizwa kurejea nyumbani, lakini hali bado si shwariMashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yametangaza kuwa, maelfu ya raia wa Burundi waliolazimika kuikimbia nchi yao hivi sasa wamo katika mashinikizo ili warejee makwao lakini hali katika nchi hiyo bado si shwari.
Wakimbizi wa Burundi wakiwa nchini Tanzania
Mashirika hayo ya kimataifa haki za binadamu yanasema kuwa, raia hao wanaoshinikizwa kurejea Burundi wanakabiliwa na kifo, mateso na vitendo vya ubakaji.
Kuna anga ya woga na hofu iliyotanda Burundi ikiwa imepita miaka miwili tangu Rais Pierre Nkurunziza alipobadilisha Katiba na kisha kushinda kiti cha Urais katika uchaguzi uliolalamikiwa ndani na nje ya nchi hiyo, imeeleza taarifa hiyo ya mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu.
Zaidi ya raia laki nne wa Burundi wameikimbia nchi yao wakihofia usalama wa maisha yao tangu Aprili mwaka 2015 wengi wao wakiwa wamekimbilia katika nchi jirani za Tanzania, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mwezi uliopita, Tanzania, Burundi na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR walikubaliana kwamba kufikia mwisho wa mwaka huu wawe wamewarejesha wakimbizi elfu kumi na mbili wanaoishi Tanzania. Wakimbizi hao ni wale wanaotaka kurejea nchini kwao kwa hiari.
Ripoti ya shirika hilo inaeleza kuwa, hali ya usalama  nchini Burundi bado sio shwari na kwamba, bado kungali kuna visa na matukio ya kuteswa, kuwekwa kizuizini bila ya hatia, ubakaji na hata kuuawa. Hata hivyo serikali ya Burundi imekuwa ikikana ripoti za kuweko ukiukaji wa haki za binadamu katika nchi hiyo na kueleza kwamba, ripoti hizo zina matashi ya kisiasa.
Parstoday
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment