Saturday, October 7, 2017

Umoja wa Mataifa: Zaidi ya watoto 8,000 wameuawa mwaka jana

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, zaidi ya watoto elfu nane wameuawa au wamepata majeraha makubwa katika mwaka uliopita wa 2016 kutokana na vita na mapigano ya silaha katika maeneo mbalimbali duniani.
Umoja wa Mataifa umetangaza katika ripoti yake hiyo kwamba, kuna nchi ambazo zimehusika katika mauaji hayo na kwamba, Saudia imo katika orodha hiyo nyeusi.
Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa, hujuma na mashambulio dhidi ya watoto hayakubaliki hata kidogo na kwamba, yanatisha mno. Katibu Mkuu huyo amezitaka pande zilizomo katika vita zisiwaingize vijana wadogo katika vita.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa nchi ambayo imeshuhudia maafa zaidi dhidi yya watoto ni Afghanistan ambapo watoto 3,512 waliuawa mwaka uliopita. Aidha nchini Yemen watoto 1,340 na nchini Syria watoto 1299 waliuawa mwaka jana katika hujuma na mashambulio tofauti katika nchi hizo.
Mamia ya watoto wengine waliathirika kwa namna tofauti kutokana na shule zao kushambuliwa kwa mabomu au kukabiliwa na ukatili wa kijinsia. Mbali na Saudia, kuna wanamgambo au wanajeshi wa Afghanistan, Jamhuri ya Afrika ya Kati,Iraq, Congo Brazzaville, Mali, Myanmar, Somalia, Sudan, Syria na Sudan Kusini ambao nao pia wamewekwa kwenye orodha hiyo ya wakiukaji haki za watoto.
Itakumbukwa kuwa, mwaka jana Umoja wa Mataifa uliiweka Saudia katika orodha hiyo nyeusi ya wakiukaji wa haki za watoto lakini Katibu Mkuu wa wakati huo wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon akaiondoa kwenye orodha hiyo baada ya Saudia kutishia kukata misaada yake ya kifedha kwa taasisi hiyo.
Parstoday 
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment