Writen by
sadataley
2:30 PM
-
0
Comments
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka
watumishi wa umma nchini wawe wabunifu katika kusaidia kutafuta vyanzo
vya mapato kwenye jamii inayowazunguka.
Ametoa wito huo leo (Jumanne, Februari
14, 2017) ofisini kwake mjini Dodoma mara baada ya kupokea mchango wa
sh. milioni 5.6 kwa ajili ya kununulia madawati 70 kutoka kwa watumishi
wa TAMISEMI – Dodoma.
Amesema ubunifu huo uliofanywa na
watumishi wa TAMISEMI, ni mfano mzuri wa kuigwa na watumishi wengine
nchini kwani utaisaidia Serikali kuleta maendeleo.
“Hii ni mara ya tatu kwa TAMISEMI
kuchangia huduma za jamii kwenye maeneo mbalimbali nchini… lakini pia
niwashukuru kwa kuchagua jimbo la Ruangwa kuwa miongoni mwa maeneo
ambayo ni wanufaika wa mchango wenu,” amesema.
“Mchango huu ni mkubwa na utasaidia
mikondo miwili kwa shule za sekondari. Tunahitaji kupata mawazo mapya
kama haya, na tunahitaji wafanyakazi wengine wajifunze kutoka TAMISEMI,”
amesema.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi
mchango wao, kiongozi wa ujumbe ulioenda kuwasilisha mchango kwa Waziri
Mkuu, Bw. Filbert Rwakilomba amesema lengo lao ni kuchangia madawati 100
lakini wameamua kutanguliza mchango wa madawati 70 na baada ya siku
mbili watakabidhi mchango wa madawati 30 yaliyobakia.
Bw. Rwakilomba ambaye anaongoza kamati
ya watu 30 ambao ni watumishi kutoka idara tofauti za Ofisi ya Rais
TAMISEMI Dodoma, amesema wametoa mchango huo kama ishara ya kuenzi kazi
aliyoifanya Waziri Mkuu Majaliwa wakati akiwa Naibu Waziri (TAMISEMI –
Elimu).
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMANNE, FEBRUARI 14, 2017.
No comments
Post a Comment